07/06/2026
KUWA NA SUBRA EWE MGONJWA
Ndugu yangu mgonjwa, usikate tamaa kwa hali unayopitia. Maradhi ni mtihani kutoka kwa Allah na ndani yake kuna kheri nyingi ambazo wakati mwingine hatuzioni. Allah Anapompenda mja Wake humjaribu ili amtakase na amnyanyulie daraja zake.
Endelea kuwa na subra, kwani kila maumivu unayoyahisi, kila usiku unaokosa usingizi kwa sababu ya ugonjwa, na kila huzuni inayokupata kutokana na maradhi yako, yote hayo Allah Anayajua na Atakulipa kwa malipo makubwa siku ya Qiyama.
Kumbuka kuwa hakuna ugonjwa ambao Allah Ameuteremsha isipokuwa Ameweka pia tiba yake. Hivyo usikate tamaa na rehema za Mola wako. Endelea kumuomba Allah, kufuata maelekezo ya madaktari na kutegemea msaada Wake katika kila hali.
Mara nyingi maradhi hutukumbusha udhaifu wetu na kuturudisha karibu zaidi na Allah. Hivyo tumieni muda huu kwa dhikri, dua, istighfar na kusoma Qur'an kadiri ya uwezo wenu. Hakika baada ya dhiki huja faraja na baada ya ugumu huja wepesi.
Dua ya kumuombea mgonjwa
اللَّهُمَّ رَبَّ النَّاسِ أَذْهِبِ الْبَأْسَ وَاشْفِ أَنْتَ الشَّافِي لَا شِفَاءَ إِلَّا شِفَاؤُكَ شِفَاءً لَا يُغَادِرُ سَقَمًا
Allahumma Rabbannasi adh-hibil ba'sa washfi Antash-Shaafii laa shifaa'a illaa shifaa'uka shifaa'an laa yughaadiru saqamaa
Maana yake:
"Ewe Allah Mola wa watu, ondosha ugonjwa huu na umponye. Wewe ndiye Mwenye kuponya. Hakuna uponyaji isipokuwa uponyaji Wako, uponyaji ambao hauachi ugonjwa wowote."
Tunamuomba Allah Awape shifaa ya haraka wagonjwa wote, Awafute dhambi zao kupitia maradhi yao, Awajalie subra na nguvu, na Awavishe vazi la afya njema. Aamiin.
Follow Iqrah Elimu ✅